TEKNOLOGIA
DUNIA sasa ni kama kijiji ?
Ndio kwani watu wengi duniani wanatumia teknologia ya habari na mawasiliano TEHAMA(ICT)
JE KUNA FAIDA GANI ZA KUTUMIA TEHAMA NA ZIPI HASARA ZAKE?
ONGEZEKO la Matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) kote duniani, hakuna anayebisha kuwa kumetokana na kupanuka na kushamiri kwa utandawazi ambapo ndani yake hata hivyo, kuna faida na hasara zake.
Pamoja na kuwepo hasara, faida ziko nyingi kwa sababau kunaisogeza dunia kuwa kijiji kwa maana ya kurahisisha mawasiliano yanayotuwezesha kupata taarifa na habari mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kisiasa, mazingira na utamaduni kwa urahisi na kwa muda mfupi.
Kutokana na uwezo wa teknolojia hii, elimu pia huweza kutolewa kwa njia hiyo na ndivyo wanavyolazimika kuitafuta baadhi ya watu, lakini pia kuna walakini fulani iwapo inakuwa tegemezi kuliko ile ya darasani kwa mtu anayelenga kuendelea zaidi kimasomo.
Hilo limejidhihirisha nchini Niger, ambako idadi kubwa ya wanafunzi katika elimu ya Sekondari na elimu ya juu wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wenye sifa katika ufundishaji na utoaji elimu.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, wanafunzi wengi nchini humo hulazimika kumiminika kwa wingi katika vituo vya huduma ya intaneti kupata mahitaji ya masomo yanayopatikana kupitia mitandao mbalimbali.
Pamoja na kukimbilia kwa wanafunzi hao katika vituo hivyo, walimu nchini humo wanatilia shaka mfumo huo mpya wa kujifunza, kwamba pamoja na mambo mengine unaathiri uhusiano kati ya wanafunzi na walimu hao.
Teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano licha ya ubora wake na kurahisisha upashanaji habari umeingilia maisha ya kundi kubwa la wanafunzi nchini humo.
Tangu kufunguliwa kwa kituo cha Francophone mwaka 2005 katika taifa hilo la Afrika Magharibi kumekuwa na ongezeko la kasi la vituo vya huduma za Intaneti kwani miji yote mikubwa na vitongoji vyake imesheheni huduma hiyo.
Wanafunzi wa shule na vyuo vikuu wameathiriwa na aina hiyo mpya ya kusoma na kupata maarifa na mafunzo kupitia mitandao kiasi kwamba huwa hawakosekani katika vituo hivyo mchana kutwa, usiku kucha.
Wanafunzi hao ambao wengi wao ni vijana hutumia muda mwingi katika vituo hivyo bila kuchoka wakiperuzi kupata taarifa wanazolenga ili kukamilisha kozi zao na kufanya mazoezi (Home work) walizoachiwa na walimu wao.
"Idadi ya wanafunzi hao inaongezeka kila kukicha"anathibitisha Amadou Moussa, msimamizi katika kituo kimoja cha Intaneti katika moja ya vitongoji kuzunguka mji mkuu wa nchi hiyo, Niamey kwa zaidi ya miaka mitano.
Baadhi ya wanafunzi katika vituo vya intaneti hawalali, wanakesha na hawakosi kufika hata siku moja katika vituo hivyo, kusaka taarifa muhimu katika mitandao hiyo.
"Intaneti haina ukomo, ni chanzo na kisima cha maarifa kisichokaukiwa na habari kwa masomo ya kawaida na yale ya Sayansi. Naangalia na kufanya mazoezi ya hesabu na mengine kila siku asubuhi"anasema Ali Ibrahim, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo ya Sayansi katika kituo kimoja cha Intaneti mjini humo.
Sauti pekee unayoweza kuisikia ni milio ya ‘hard disks’ na ‘keyboard’, wanafunzi wanaonekana wakipitia somo lao la Fizikia na macho yao yakiwa yameelekezwa mbele ya ‘skrini’ ya kompyuta wakionekana kufurahia hali hiyo.
Kuperuzi katika kompyuta huwasaidia wanafunzi hao kupata matokeo mazuri na kujiandaa kwa mitihani yao ya mwisho.
Aina hiyo ya kujifunza ni rahisi, ni kiasi cha kuperuzi katika eneo la kutafutia taarifa (Search) huru.
Wanafunzi katika vituo hivyo, hutozwa kiasi cha fedha kisichopungua nusu dola ya Kimarekani kugharamia huduma hiyo.
Pamoja na ubora na kushamiri kwa huduma hiyo na kusaidia utoaji wa elimu kwa wanafunzi nchini humo kupitia teknolojia ya kisasa ya habari na mawasiliano, bado njia hiyo haitoi jibu na matarajio ya moja kwa moja katika kupata elimu.
"Njia hii ina athari kubwa ya uhusiano kati ya wanafunzi na walimu wao"alionya Chaibou Boucarar, mwalimu wa fasihi nchini humo.
Hali hiyo imesabisha wazazi wengi nchini humo kuwanyoshea vidole viongozi wa Taifa hilo wakidai kuwa ndio wakutupiwa lawama kutokana na hali hiyo.
Katika kipindi cha miaka 10, mfumo wa elimu nchini Niger umekabiliwa na migomo toka pande zote walimu na wanafunzi.
Idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma elimu ya Sekondari nchini humaliza masomo hayo bila kukamilisha silabasi iliyowekwa sambamba na masomo hayo.
Hali hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na utaratibu wa nchi hiyo kwa walimu hao kufanya kazi kwa mkataba mfumo unaolalamikiwa na wadau wa elimu nchini humo.
Walimu nchini humo kutoandaliwa vyema na ukosefu wa vitendea kazi na vifaa vya kufundishia.
Mishahara midogo na isiyokidhi haja, motisha na ukosefu wa utaratibu na muuundo mzuri wa kuwaendeleza walimu ni kati ya sababu inayosababisha hali hiyo ya malalamiko ya walimu na wadau hao wa elimu nchini humo.
Wizara ya elimu nchini humo inalalamikiwa na walimu, wanafunzi na wadau wa elimu kwamba inaangalia zaidi na kutilia mkazo katika utoaji elimu badala ya kuzingatia ubora wa elimu hiyo.
Kitendo cha wanafunzi kutafuta taarifa mbalimbali kwenye Intaneti ni ushahidi wa tatizo hilo, anasisitiza mwalimu wa somo la elimu ya viumbe (Biology) Abdou Hassan.
Licha ya kusaidiwa kupata taarifa toka kwa wahudumu katika vituo hivyo, baadhi ya wanafunzi hukaa pekee yao mbele ya kompyuta na kupata habari.
Lakini wakati mwingine wanafunzi watukutu hutumia huduma hiyo muhimu katika kuangalia na kuona picha zisizofaa ambazo huathiri utamaduni, mila na desturi za Kiafrika
No comments: